Wapendwa vijana kutoka nchi mbalimbali Duniani,
Kuanzia tarehe 26-30 Novemba mwaka huu, tunawakaribisha hapa Kenya katika tukio maalum la maombi, kushirikishana, kutafakari na tunawaalika katika makanisa mbalimbali katika jiji letu la Nairobi.
Mabruda kutoka Taize wamekuwa kwenye maandalizi ya mkutano huu katika vipindi mbalimbali vya mwaka jana. Miaka iliyopita vijana wa Kenya wametembelea Taize mara nyingi, hasa wakati wa kiangazi, kushiriki mikutano ya kimataifa iliyofanyika katika vilima vya Burgundy. Sasa ni zamu yetu kukukaribisheni!
Sura zetu si ngeni kwa baadhi yenu, tulikuwepo Geneva mwezi January mwaka huu kwenye mkutano wa Ulaya. Katika sala mojawapo tukiwa na Br Alois tulitoa tangazo la mkutano huu wa Nairobi, tuliporudi nyumbani tulianza mikakati na kazi za maandalizi.
Kama mjuavyo mkutano huu wa Nairobi umekuja katika kipindi cha kihistoria kwa Kenya, nchi kubwa ambayo tangu uhuru wake mwaka 1963, imekuwa ikipambwa na tamaduni mbalimbali. Kauli mbiu ya mkutano huu; ni muafaka “Pamoja tukitafuta njia za matumaini”, sisi vijana wa Kenya tunatambua alama za matumaini ambazo tayari zipo katika jamii na kanisa, tunawaasa nyote (pamoja nawe) kuwa wajumbe wa Ukweli katika mazingira ambayo Mungu hutuweka siku hadi siku.
Mnapojiandaa kuja Nairobi, mtashangaa kuonana na watu wakarimu wenye shauku kubwa ya kuwakaribisheni kwenye nyumba zao na kuwakirimu kwa kidogo walichojipatia katika hali ngumu. Mtashuhudia furaha yao na kujitoa kwao katika makaribisho yenu. Mfikapo kwenye familia pokeeni kwa unyenyekevu mtakachopewa, kuwaenzi wageni na kuhakikisha wanajitosheleza ni msingi wa jamii yetu, tunajiaandaa mapema kuwakaribisha wageni na kutoa vilivyo bora kwao na tunavunjika moyo vinapokataliwa.
Karibuni sana Nairobi, Kenya