TAIZÉ

Thamani ya ukimya

 
Mara tatu kila siku, kila kitu husimamishwa kwenye kilima cha Taizé: kazi, masomo ya biblia, majadiliano katika vikundi vidogo vidogo. Kengele zinaita kila mmoja kwenda kanisani kwa ajili ya sala. Mamia, na wakati mwingine maelfu ya vijana kutoka nchi nyingi ulimwenguni wanasali na kuimba pamoja na mabruda wa jumuiya. Biblia husomwa katika lugha mbalimbali. Kipindi cha ukimya hutawala kwa muda katikati ya sala, ambacho hutoa fursa ya pekee kabisa na ya aina yake ya kukutana na Mungu.

Ukimya na sala

Kama tunachukua vitabu vya zamani kabisa vya sala na zaburi kama mwongozo wetu, tunaona aina mbili za sala. Mojawapo ni sala za majuto na kuomba msaada, nyingine ni sala za kushukuru na kumsifu Mungu. Katika hali ya kufichika zaidi, kuna aina ya tatu ya sala, isiyo na maombi au muonekano wa waziwazi wa kusifu. Kwa mfano katika zaburi ya 131, hakuna kitu isipokuwa utulivu na kujiamini: “nimejishusha kabisa na kutuliza nafsi yangu… namtumainia Mungu tangu sasa na milele”

Wakati fulani sala inakuwa kimya. Ushirika wa amani na Mungu unaweza kufanyika bila kutamka maneno. “nimejishusha na kutuliza nafsi yangu, kama katoto kadogo kaliko achishwa kunyonja kakiwa na mama yake.” Kama katoto kalikoridhika na kunyamaza kulia na kako mikononi mwa mama yake, vivyo hivyo nafsi yangu yaweza kuwa” katika uwepo wa Mungu. Kwa hivyo, sala haihitaji maneno, na pengine hata mawazo.

Ni vipi basi inawezekana kupata ukimya wa ndani? Wakati fulani tunakuwa tuko kimya tu, na bado tuna majadiliano makubwa sana ndani yetu, tukipambana na wenzetu katika mawazo, au na nafsi zetu wenyewe. Kutuliza nafsi zetu kunahitaji urahisi wa namna fulani: “sijijazi na mawazo ya mambo makubwa sana au ya ajabu na kunistaajabisha sana ”. Ukimya maana yake ni kumuachia Mungu yale yote ninayoona kuwa si rahisi kwangu na yako nje ya uwezo wangu. Nyakati za ukimya, hata kama ni kwa muda mfupi, ni kama pumziko takatifu, na mwisho wa hofu.

Mkingamo wa mawazo yetu unaweza kufananishwa na dhoruba iliyopiga mashua ya mitume wa Yesu kwenye bahari ya Galilaya wakati Yesu akiwa amelala. Kama wao walivyokuwa, tunaweza tukawa watu wasio na msaada, tuliojawa na wasiwasi, na tusioweza hata kujituliza wenyewe. Lakini Kristo anaweza kuwa msaada wetu vilevile. Kama alivyokemea upepo na bahari na “kukawa na utulivu mkubwa”, anaweza pia kutuliza mioyo yetu inapokuwa imetiwa wasiwasi mkubwa. (Marko 4) Kwa kubaki kimya, tunaamini na kumtumainia Mungu. Mzaburi mmoja anapendekeza kuwa, ukimya ni namna ya kusifu. Tumezoea kusomo mwanzoni mwa zaburi ya 65: “sifa ni kwako eeMungu”. Wakati mawazo na maneno yanafikia mwisho, Mungu anasifiwa katika ukimya wa ajabu na wa kuheshimika.

Neno la Mungu: Ngurumo na kimya

Kule Sinai, Mungu aliongea na Mose na Waisraeli. Ngurumo na radi na sauti kubwa kabisa za matarumbeta zilitangulia na kusindikiza neno la Mungu. (kutoka 19). Karne kadhaa baadaye, Nabii Elia alirudi katika ule mlima wa Mungu. Hapo alisikia ngurumo na tetemeko la aridhi na moto mkubwa kama mababu zake walivyoona, na alikuwa tayari kumsikia Mungu akiongea kutoka katika hizo ngurumo. Lakini Mungu hakujiweka katika hali ya kuwa na nguvu kama ilivyozoeleka. Baada ya kelele zote kuisha, Elia alisikia “sauti mwanana katika ukimya” na Mungu akaongea naye. (1 Wafalme 19)

Sasa je, Mungu anaongea katika sauti kubwa au katika utulivu? Tuchukue mfano wa watu waliokusanyika Sinai au nabii Elia? Hii inaweza ikawa njia isiyo sahihi. Hali ya kutisha na kuogofya inayo husiana na amri kumi za Mungu inasisitiza ni kwa namna gani haya yanamaanishwa. Kuyachukua au kuyaacha ni swala la kuishi au kufa. Mtu akiona mtoto anakimbilia gari inayokuja kwa kasi, ana haki ya kupiga kelele kadiri inavyo wezekana. Kwa namna inayofanana na hiyo, manabii walizungumzia neno la mungu, ili lisikike masikioni mwetu.

Maneno yatolewayo kwa sauti kubwa ni dhahiri kusikika, na hufurahisha. Bali tunajua pia kwamba nivigumu sana kugusa mioyo. Huwa yanazuiliwa badala ya kupokelewa. Tukio la Elia linatuonyesha kuwa, Mungu hahitaji kufurahisha, ila kueleweka na kukubalika. Mungu anachagua “sauti mwanana katika ukimya” ili kuongea. Huu ni utata.

Mungu yupo mkimya na bado ana sema

Wakati neno la Mungu linapokuwa “sauti mwanana katika kimya”, ni la manufaa makubwa na laweza kubadili mioyo yetu. Ngurumo kubwa katika mlima Sinai, zilikuwa zavunjavunja miamba, lakini neno la Mungu lisilo na sauti, laweza kuvunja moyo mgumu/wa jiwe kwa mtu ambaye yuko tayari. Hata kwa Elia mwenyewe, kimya cha ghafla kilimuogofya kuliko ilivyokuwa kwa ngurumo na radi. Sauti kubwa na uweza na nguvu za Mungu, zilikuwa si kitu kigeni kwake. Kimya cha Mungu kina muogofya na kumtisha Elia, kwa namna ya tofauti sana na alivyokuw anajua kabla. Kimya kinatufanya kuwa tayari kukutana na Mungu.

Katika ukimya, Neno la Mungu laweza kufikia pembe zote za moyo zilizojificha. Katika ukimya, Neno la Mungu linakuwa “kali kupita mkuki wenye pande mbili, likichoma na kupenya hadi kugawanya nafsi na roho”. (waebrania 4:12). Katika ukimya tunaacha kujificha na Mungu, mwanga wa kristo waweza kutufikia na kutuponya pia kutugeuza hata kwa yale tunayoonea aibu.

Kimya na upendo

Yesu anasema: “amri yangu ni hii, kwamba mupendane kama mimi nilivyo wapenda ninyi” (yohane 15:12). Twahitaji ukimya ili kuweza kupokea maneno haya na kuyaweka katika vitendo. Tukiwa na hasira na hali isiyo ya utulivu, tunakuwa na sababu nyingi sana za kutosamehe, na kutowapenda wengine kirahisi. Lakini tukiwa “tumetulia na kutuliza nafsi zetu,” sababu hizi zinageuka kuwa zisizo za maana wala muhimu tena. Labda wakati mwingine hatupendi ukimya, tukipendelea kelele za aina yoyote, maneno au vitu vinavyokufanya ujisahau unafanya nini, kwa sababu amani ya ndani ni kitu kinachoweza kuwa cha hatari: inatufanya kuwa watupu na maskini, husambaratisha uchungu na kutuelekeza kwenye furaha. Katika ukimya na hali ya umaskini, mioyo yetu imejazwa na roho mtakatifu, na upendo wa kweli usiokuwa na masharti. Ukimya ni upole na hapo hapo njia nzuri ya kuwa na upendo.

Ilirekebishwa mara ya mwisho: 14 August 2007